SERIKALI YA KAUNTI YA TURKANA

HOTUBA YA MHESHIMIWA JOSPHAT KOLI NANOK

GAVANA WA KAUNTI YA TURKANA WAKATI WA SHEREHE ZA SIKU KUU YA JAMHURI TAREHE 12 DISEMBA 2014, MJINI LODWAR.

 

Naibu wa Gavana,

Mhemishimiwa Senator,

Kamishina wa Kaunti,

Mheshimiwa Spika   wa Bunge la Kaunti,

Maafisa Wakuu wa Serikali ya Kaunti ,

Waheshimiwa Wabunge la Kaunti ,

Waheshimiwa Wabunge la Kitaifa ,

Wananchi watukufu wa kaunti ya Turkana,

 

Mabibi na Mabwana:

Nawasalimu nyote na kuwakaribisha kwa siku kuu hii ya Jamhuri .

Kwa mara nyingine leo hii, tunaadhimisha na kusherehekea siku muhimu ya  miaka 51 ya uhuru wetu kutoka kwa Wakoloni.  Ni siku ya kutoa heshima na kuwaenzi waanzilishi wa taifa hili kwa moyo wao mkuu, ushupavu na azima kwa maono- maono ambayo hatimaye yalisaidia kupatikana kwa uhuru  wa nchi na makao ya mashujaa.

Bila shaka tunaadhimisha siku kuu ambayo ina baraka maradufu kwetu Wakenya.  Hii ni siku ambayo tulipata uhuru wetu kutoka kwa Waingereza mwaka wa 1963 na mwaka mmoja baadaye 1964 Kenya ikasajiliwa kama mwanachama wa Jumuiya ya Madola na vile vile katika Umoja wa Mataifa kama  taifa linalojitawala.

Mabibi na Mabwana:

Siku kuu ya Jamhuri sio tu siku ya kutafakari; ni siku ya kutoa heshima na  kuonyesha shukrani zetu kwa uhuru wetu tulio nao hadi wakati huu. Ni siku ya kutazamia nyakati zijazo zenye nafasi tele zinazostahili kutumiwa na kuafikiwa.

Kwetu sisi katika  Kaunti hii, ni siku ya kushikana mikono na kuungana kuifanya  Kaunti hii kuwa bora zaidi kwa kizazi hiki na vizazi vingi vijavyo.

Mabibi na Mabwana:

Hadithi  ya Turkana imebadilika, hatutaendelea kurudia wimbo wa kupuuzwa na kutengwa ambako tulipitia kwani sasa hayo ni ya kale.  Tumejikwamua na kuamua mwelekeo wa maendeleo yetu.

Ni karibu miaka miwili sasa tangu mnipe jukumu la uongozi kama Gavana wenu na wale wanaofahamu wanaweza kushuhudia yale ambayo serikali  imeafulu kutimiza katika muda usiozidi miaka miwili. Ni ombi langu kwamba kila mwaka, utakuwa mwaka wa mafanikio kwa kaunti ya Turkana.

Mabibi na Mabwana:

Hali ya ukosefu wa usalama:

Kaunti yetu inaendesha vita hatua kwa hatua na kwa umakinifu dhidi ya viwango vya juu vya umaskini, ukame, kutokuwepo kwa usalama na kutojua kusoma na kuandika. Moyo wetu wa kijamii, ufungamano na  matarajio ya pamoja ni thabiti na unaweza kukabiliana na  changamoto zinazotukumba wakati huu za kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Hali mbaya ya usalama imeendelea kuwa changamoto kali kwetu katika kaunti hii. Eneo la mpaka kati ya Kaunti ya Turkana na Pokot Magharibi limeendelea kukumbwa na matatizo mengi.

Tumepoteza watu wengi kutokana na  majambazi kutoka Kaunti hizi mbili. Hali hii lazima ikome. Hii ndio sababu tunaiambia serikali ya kitaifa ishirikishe kaunti katika jukumu la usalama. Iwapo itahitajika kurekebisha katiba ili kuruhusu kaunti kushirikishwa katika masuala ya usalama basi na iwe hivyo. Na iwapo serikali ya kitaifa imegundua haitaweza kushughulikia usalama wa ndani bila kushirikisha serikali za kaunti na raia wake basi tutaunga mkono msimamo huo.

Ikiwa serikali ya kitaifa imefaulu kuwaafikia jirani zetu Sudan Kusini na kutumia majeshi kuleta amani nchini Somalia, je itakuwaje eti imeshindwa kukabiliana na majambazi  na wezi walioko nchini? Hii ni kile ninachosema kuwa upungufu katika mfumo wa utaratibu wa vikosi vyetu vya usalama. Marekebisho katika mfumo wa usalama sharti yapewe kipau-mbele katika kaunti yetu na pia katika sehemu zote za nchi yetu.

Mabibi na Mabwana:

Huku mjadala kuhusu usalama ukiendelea, serikali yangu itaendelea kufanya kila iwezalo kuhakikisha watu katika maeneo ambayo si salama wanapata usalama wanaposafiri. Mojawapo wa juhudi hizi ni kutengwa kwa shilingi milioni 100 kwa ujenzi wa daraja la  Kaputir ambalo litarahisisha kuchukuliwa kwa hatua ya haraka kuwashughulikia watu walioko ukingo wa magharibi.

Serikali yangu pia imetenga fedha kuwalipa maafisa wa polisi wa akiba

(KPR) ambao wakati huu wanatambulika kama Maafisa wa polisi wa  Kitaifa wa  akiba  (NPR) kuchangia kazi ya maafisa wa usalama wa kitaifa katika kaunti.

Mabibi na Mabwana:

Kandarasi za Utendaji kazi:

Nilipochukua hatamu za uongozi, niliahidi  kutoa huduma kwa watu wa Turkana; serikali yangu itaendelea kujitolea kwa kazi hii, Majuma mawili yalioyopita, Wakuu wote wa Kaunti walitia saini Kandarasi za Utendaji Kazi, kuonyesha kujitolea kwao kwa kazi na  kushinikizwa na  hatua hiyo katika utoaji huduma kwa watu wa Turkana.

Hii ni hatua bora iliyochukuliwa na serikali sio tu kwa kuhakikisha utoaji huduma bora bali pia kufuatilia utendaji kazi katika idara zote za Kaunti na wafanyakazi wote.

Kandarasi za kazi zilizotiwa saini na maafisa wakuu pia zitasambazwa chini kwa kila mfanyakazi wa serikali ya kaunti kama ishara ya nia ya kibinafsi  ya kutoa huduma.

Hatua hii inambana kila mmoja na kumfanya kuwajibika mwisho wa kila kipindi cha  mwaka wa matumizi ya pesa za serikali kwa kile walichofanya na kile walichoshindwa kutimiza, na umma  utakuwa hapo kuwakadiria.

Mabibi na Mabwana: 

Huduma za Afya:

Usajili wa hivi majuzi wa wahudumu wa afya, tuliajiri wafanyakazi wa afya 306 ambao watapelekwa katika vituo vya afya vilivyokamilika na ambavyo vimejengwa na serikali. Serikali yangu inakusudia kuwa na  zahanati mbili katika kila wadi ili kupunguza dhiki.

Katika wahudumu hao wa afya 306, tulikuwa na wanawake 158 na wanaume 148, hivyo basi hatua hii inakuonyesha kwamba serikali yangu inamakinika kuwapa nafasi wanawake.

Mabibi na Mabwana:

Muundo Msingi:

Malengo yangu ni kuhakikisha kuna barabara nzuri  zinazounganisha sehemu zote katika kaunti hii kwani hatua hiyo itarahisisha usafiri wa kila mmoja na kupunguza masaa ya kusafiri na vile vile kuongeza ustaraabu kwa watu wetu.

Mwaka huu tunakusudia kutengeneza barabara nne, ambapo kazi tayari imeanza katika baadhi ya sehemu za kaunti hii. Ujenzi wa kilomita sita tuliozindua unaendelea, vile vile kazi ya ujenzi wa mitaro ya kuondoa maji taka na kuwekwa kwa taa za barabarani kunaendeshwa kwa njia nzuri.

Mabibi na Mabwana:

Maji

Serikali yangu inatengeneza mswaada kuhusu maji unaokusudiwa kuimarisha huduma za maji katika Kaunti. Huduma za maji zitafadhiliwa na kusimamiwa na serikali ya kaunti.

Mswaada huu utaiwezesha kaunti kutoa bili za maji kupitia mitambo ya tarakilishi ili kuzuia wizi wa maji na vile vile itasaidia kupunguza gharama za huduma za maji.

Mabibi na Mabwana:

Elimu:

Serikali yangu inathamini elimu kwa watoto wetu. Nilipochukua hatamu za uongozi nilitangaza vita dhidi ya kutokujua kusoma na kuandika. Hivyo basi, nimeongeza kiwango cha fedha zinazotumiwa kwa hazina ya misaada ya masomo kutoka kiwango cha wakati huu cha  shilingi milioni 150 hadi shilingi milioni 342 .

Hivyo basi, nawahimiza wazazi wote wawapeleke watoto wao shule ili wanufaike na mpango huo.

Mabibi na Mabwana:

Kujitosheleza kwa  Chakula:

Hata ingawa serikali yangu inachukua mwelekeo wa kilimo cha unyunyizaji maji mashamba, mpango  wa dharura pia ni muhimu, hivyo basi, serikali yangu inapanga majira ya kutoa misaada ya chakula cha dharura kwa zaidi ya watu 500,000. Vile vile, tunapanga kuanzisha mpango wa kusambaza shilingi milioni 150 katika mpango utakaowanufaisha watu 18,900.

Mabibi na Mabwana:

Biashara:

Serikali yangu imetenga  milioni 60 kwa hazina za biashara ndogo-ndogo na za kadri. Hazina hii inakusudiwa kuwawezesha na kuwahimiza watu wa sehemu za wadi kuomba mikopo  kwa masharti nafuu ili kuimarisha biashara zao. Vile vile, nimetenga shilingi milioni 30 kwa vyama vya ushirika.  Tutaanzisha mpango huo mara tu miswaada  miwili ambayo iko tayari  itakapopitishwa katika utaratibu unaohitajika na kuidhinishwa na Bunge la Kaunti.

Serikali yangu pia inazindua mpango wa ujenzi wa soko la kisasa katika kila wadi.  Tayari ujenzi wa masoko mawili kama hayo unaendelea huko Lokori na Nakurio.

Ukarabati wa soko la Lodwar sasa umekamilika na soko hilo litakabidhiwa wafanyabiashara hivi karibuni. Ninatambua kwamba huenda soko moja halitoshi na hivyo kutajengwa soko lingine la pili la kisasa hapa Lodwar.

Mabibi na Mabwana:

Utalii

Serikali yangu imeanzisha utaratibu wa kupiga rajamu na kutangaza Kaunti hii kama kivutio cha kitalii. Rajamu au alama yetu kubwa ni ufahamu wa kisayansi wa chanzo cha Mwanadamu. Turkana ni mahali mwanadamu alianzia,  hii ndiyo alama yetu. Ili Kuunga mkono ukweli huu ambao   bila shaka umethibitishwa kisayansi, serikali yangu ikishirikiana na Richard Leakey, Taasisi ya Ziwa Turkana zinashauriana kwa kina kujenga makavadhi kubwa zaidi mjini Lodwar ambayo yatakuwa makavadhi kubwa mno ulimwenguni.

Hivyo basi, Serikali yangu pia imeanzisha ujenzi wa nyumba mbili za utalii wa viumbe na mazingira huko  Kainuk na Kataboi kila mojawapo ikiwa na uwezo wa kuhudumia watalii 40 wa kulala. Serikali yangu inashirikiana na  Chuo cha Utalii kuimarisha uwezo wa wahudumu wa hoteli na kuboresha viwango vya huduma katika sekta hiyo. Tayari watu 72 kutoka kwa kaunti hii wamenufaika na mpango wa mafunzo haya. Mpango wetu mwishowe ni kwamba tuwe na nafasi zinazotengwa katika chuo cha Utalii kwa wale wanaokusudia kujiunga na  sekta ya ukarimu na wako tayari kurejea na kuekeza hapa nyumbani.

Mabibi na Mabwana:

Mkutano wa wafadhili na washirika tuliofanya katika ufuo wa Ziwa Turkana umeanza kuzaa matunda. Waekezaji wameonyesha nia kubwa ya kuunga mkono miradi hapa Turkana. Umoja wa Mataifa umetangaza  msaada wake  katika  kuafikia mpango wetu wa Ushirikishi wa Maendeleo ya Kaunti

Vile vile, tumepata msaada kutoka  kwa shirika la maendeleo ya kimataifa la Uingereza-DFID kuhamasisha umma kuhusu masuala ya mafuta na gesi. Hii ni muhimu kwa ushirikishi wa umma tunapoingia awamu ya  uchimbaji mafuta katika kaunti.

Mabibi na Mabwana:

Fedha:

Hii ndio kaunti ya  pekee nchini ambayo imetenga aslimia kubwa ya mapato yake kwa maendeleo. Kwa wakati huu matumizi yetu ya aslimia 30 yanaelekezwa kwa shughuli za kila siku ilihali aslimia 70 imetengwa kwa maendeleo. Huu ni mwelekeo unaofaa.

Fedha tulizotenga kwa maendeleo katika kipindi cha mwaka huu cha matumizi ya pesa za serikali ni  shilingi bilioni 9.1 ikiongezwa na  shilingi bilioni 3.8 zilizowasilishwa kutoka mwaka uliopita wa matumizi ya pesa za serikali. Hatua hii inatupatia  shilingi bilioni 12.9 ambapo shilingi bilioni  3.5 tayari zimetumika na kiasi kingine cha shilingi bilioni tatu kutengwa kwa miradi ambayo kandarazi yao imeshapeanwa.

Tunachopaswa kujua ni kwamba kiasi kikubwa cha bajeti yetu kinatumika kwa maendeleo na kila wakati pesa zinapochelewa kutolewa na hazina kuu, kiwango cha matumizi pia kinaathirika, hii haimaniishi eti kwamba pesa zilizosalia  zinarudishwa.

Hatuna la kuficha kama serikali; utaratibu wa bajeti ni wa wananchi. Tutaendelea kuwa wazi na kuwajibikia watu wa Turkana. Uwazi na hadhi ndio kanuni zinazozingatiwa na serikali yangu.

Mabibi na Mabwana:

Tunajenga  kaunti yetu kuanzia muundo msingi na kwa niaba ya serikali ya kaunti; tujajitolea kuhudumia kaunti hii tukufu. Ni heshima yangu kuthibitisha kwamba haijalishi changamoto zinazotukumba, tupo katika njia sawa kuufikia ukuu. Ajenda yetu ya maendeleo, ambayo ni sehemu ya maono yetu makuu ya  kuifanya kaunti ya Turkana kuwa   eneo kuu yanaleta matokeo bora na ya kutia moyo.

Nachukua fursa hii kumtakia kila mmoja Krismasi njema na Mwaka mpya wa Furaha na Mafanikio wa 2015.

 

Tujivunie Kaunti yetu na Urithi wetu kama jamii.

 

Siku kuu njema ya Jamhuri !!

 

 

Comments (870)

Leave a Reply